USHUJAA
Napuliza parapanda, kwa machungu nikilia,
Nalilia njia panda, nimeshindwa kutulia,
Maisha yamenishinda, kiti moto nakalia,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Wapiganapo fahari, nyasi ndizo huumia,
Natangazeni hatari, sikizeni mtajua,
Punguzeni zenu shari, nazo vita tapungua,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Sisi sote ni wakenya, hilo ndo letu kabila,
Lugha yetu ya kikenya, twaijua kama sala,
Viongozi nawaonya, hatutaki ukabila,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Taifa letu ni moja, na serikali ni moja,
Katiba yetu ni moja, Raisi wetu mmoja,
Uchaguzi unaokuja, usituvunjie umoja,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Matusi kurushiana, huo sio USHUJAA,
Na mawe kutupiana, ni aibu twajitia,
Epukeni kupigana, na mkae mkijua,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Lisikia redioni, vita kati ya wabunge,
Tukaona runingani, mangumi kwenye bunge,
Na juzi mkutanoni, lipigana na seng'enge,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Futina SI USHUJAA, na Wala sio silaa,
Nayo chuki ni balaa, iletwayo na tamaa,
Wachaneni na tamaa, itawaletea njaa,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Elfu mbili na saba, sisi sote tulilia,
Na hata mama na baba, tulilia nao pia,
Twauogopa msiba, mwakani kujirudia,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Wapendwa wanasiasa, tunawapa ushauri,
Uongozi wa anasa, husababisha hatari,
Uongozi wa kisasa, SI mchezo wa kamari
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Mheshimiwa raia, KAZI kubwa Iko kwako,
Ni wewe utaamua, atakayekuwa wako,
Kura yako ndo silaa, spesheli ngao yako,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Ukitaka kula nyama, kaa na wanaokula,
Ukikaa kutazama, ni mate tu utakula,
Utaishi kulalama, ili hali umelala,
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Jamvi langu kikunjeni, nawapeni ushauri,
Walioko safarini, wameketi kwenye gari,
Aliyeko kituoni, ni makanga hasafiri
USHUJAA sio vita, Bali, ni maendeleo.
Sylvester Timothy
©Platypus Writers
USHUJAA
Written on 29/07/2026
Sylvester Timothy

