Huyu punda tumtunze, tusije tukajutia.

Written on 27/07/2026
Malenga Mbarikiwa: MICHAEL IMANI ODUOR,


Huyu punda tumtunze, tuzije tukajutia.

Sikizeni wafugaji, kwa makini pulikeni,
Hili kweli nataraji, mutalitia bongoni,
Punda kwetu ni mtaji, wa kuleta nyingi peni,
Huyu punda tumtunze, tuzije tukajutia.

Kila siku kukikucha, twapata nyingi habari,
Nyama zao mnaficha, pasi kujua hatari,
Mnazua nyingi picha, kwa kuwapiga kabari,
Huyu punda tumtunze, tusije tukajutia.

Viboko tele apata, huyu punda masikini,
Ngozi mnakatakata, kichwani hadi kwatoni,
Mnazo kweli sakata, nyama haramu sokoni,
Huyu punda tumtunze, tusije tukajutia.

Mizigo mwamubebesha, asubuhi na jioni,
Jamani mnamchosha, hamuoni hata soni,
Tabia hino yatisha, mijini na mashambani,
Huyu punda tumtunze, tusije tukajutia.

Ngozi yake mnachuna, eti viatu mwataka,
Hihohiho anaguna, punda sasa anamaka,
Huyu punda ananuna, kwa yenu mengi mashaka,
Huyu punda tumtunze, tusije tukajutia.

Punda mnyama mzuri, tena mwingi wa upole,
Hili kwangu sio siri, tangu jana na milele,
Masikini na tajiri, awapa faida tele,
Huyu punda tumtunze, tusije tukajutia.

Ni vizuri tukumbuke, ni jambo lenye busara,
Ukweli ufahamike, punda anazo tijara,
Kamwe tusibabaike, tusimameni imara,
Huyu punda tumtunze, tusije tukajutia.

Ni letu sote jukumu, kumtunza punda wetu,
Mepesi ama magumu, faida bado ni yetu,
Tuipuke hukumu, kutoka kwa Mola wetu,
Huyu punda tumtunze, tusije tukajutia.

Beti tisa ninafunga, nimesema ndani nje,
Sheria tumezitunga, mbona sasa tuzivunje,
Punda wako kumchunga, wala wewe 'simchinje,
Huyu punda tumtunze, tuzije tukajutia.

 

MALENGA MBARIKIWA: MICHAEL IMANI ODUOR,
MAVOKO, MACHAKOS - KENYA.

Image source: Joaquin Reyes Ramos